Na Victor Abuso
Vlabu vya soka Gor Mahia na AFC Leopards vinashuka dimbani jioni hii kumenyana katika mchuano muhimu wa mzunguko wa pili kuwania taji la ligi kuu nchini Kenya.
Mchuano huu unaochezwa katika uwanja wa taifa wa Nyayo jijini Nairobi ni muhimu kwa vlabu vyote viwili ambavyo vina historia ya kipekee katika soka la Kenya.
Watani hawa wa jadi, wanaweka kando changamoto zao za kifedha na kutunishana misuli ili kutafuta bingwa wa mchuano wa leo na kulinda heshima.
Mabingwa wa ligi Gor Mahia wanashuka dimbani wakiwa hawajapoteza mchuano wowote katika mechi 22 walizocheza kufikia leo kinyume na Leopards ambao wamefungwa mechi 8 na wanashikilia nafasi ya tano katika msururu wa ligi wakiwa na alama 35.
Mashabiki wa vlabu hivi viwili wamekuwa wakitamba katika mitandao ya kijamii kuwa watashinda mchuano wa leo.
Mchuano kati ya vlabu hivi viwili vyenye makao yake jijini Nairobi vimepewa jina Mashemeji Derby.
Mwezi Aprili mwaka huu, vlabu hiv viwili vilitoka sare ya bao 1 kwa 1 katika mchuano wa mzunguko wa kwanza.
Gor na AFC wamekutana mara 79 katika historia yao ya soka tangu mwaka 1968 huku Leopards wakipata ushindi mara 27 na Gor mara 22 na kutoka sare mara 30.
Gor Mahia wameshinda mataji 14 ya ligi kuu nchini Kenya huku AFC Leopards wakishinda mataji 13.