Ethiopia, Sudan, Uganda na Burundi zitawakilisha ukanda wa Afrika Mashariki na Kati katika mzunguko wa pili kutafuta nafasi ya kushiriki katika michuano ya Afrika kwa wachezaji wasiozidi miaka 20 itakayofanyika mwaka ujao nchini Zambia.
Vijana wa Ethiopia walisonga mbele baada ya kuwashinda jirani zao Somalia kwa jumla ya mabao 4 kwa 1 baada ya kucheza nyumbani na ugenini.
Sudan nayo ilifuzu baada ya kufungiwa kwa Kenya kwa sababu iliwachezesha wachezaji watano wenye umri mkubwa katika mchuano wake wa kwanza ugenini jijini Khartoum.
Burundi ilifuzu baada ya jirani yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiondoa huku Uganda ikailemea Rwanda kwa jumla ya mabao 3 kwa 2.
Ratiba ya michuano ijayo mwezi Mei na Juni:-
- Sudan vs Malawi
- Burundi vs Nigeria
- Uganda vs Misri
- Ethiopia vs Ghana.
Mataifa 14 yatafuzu katika mzunguko wa tatu na mshindi baada ya mchuano wa nyumbani na ugenini atafuzu katika fainali hizo.
Nchi nane ikiwemo, wenyeji Zambia watashiriki katika michuano hiyo itakayofanyika mwezi Februari mwaka 2017.