Kenya itashiriki katika michuano ya soka ya Afrika kwa upande wa wanawake kwa mara ya kwanza, nchini Cameroon kati mwezi Novemba na Desemba mwaka huu.
Warembo wa Harambee Starlets waliweka historia siku ya Jumanne kwa kufuzu katika michuano hiyo ya Afrika kwa sababu ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya bao 1 kwa 1 na Algeria jijini Nairobi.
Mchuano wa mzunguko wa kwanza wiki moja iliyopita jijini Algers, Kenya ililazimisha sare ya mabao 2 kwa 2.
Kenya sasa inajiunga na wenyeji Cameroon ambao mwaka 2014 walimaliza wa pili lakini pia mwaka 1991 na 2004.
Misri nayo imefuzu kwa mara ya pili baada ya kushiriki mara ya kwanza mwaka 1998 na kuondolewa katika hatua ya makundi.
Mabingwa wa mwaka 2008 na 2015, Equitorial Guinea nao wamejikatia tiketi ya kucheza katika fainali hii ambayo wamechxa mara tano sasa.
Nigeria ambao ni mabingwa watetezi na ambao wameshinda taji hili mwaka 1991, 1995, 1998, 2000, 2004, 2006, 2010 na 2014, wanashiriki kwa mara ya 12.
Afrika Kusini nayo imefuzu kwa mara ya 11 na Zimbabwe iliyomaliza nafasi ya nne mwaka 2000 itacheza kwa mara ya nne.
Mataifa haya manane yatajumuishwa katika makundi mawili, kila kundi likiwa na timu nne.
Timu mbili za kwanza katika kila kundi zitafuzu katika hatua ya nusu fainali.