Mataifa 13 tayari yamefuzu kucheza fainali ya kuwania taji la mchezo wa soka barani Afrika , michuano itakayofanyika kati ya mwezji Juni na Julai mwaka 2019 nchini Cameroon.
Hii imekuja, baada ya michuano ya kufuzu hatua ya makundi kuchezwa mwishoni mwa wiki iliyopita, katika mataifa mbalimbali.
Mataifa yaliyofuzu ni pamoja na wenyeji Cameroon, Madagascar, Senegal, Morocco, Mali, Algeria, Nigeria, Guinea, Ivory Coast, Mauritania, Tunisia, Misri na Uganda.
Mauritania imeweka historia na sasa inajiunga na Madagascar, kufuzu katika michuano hii kwa mara ya kwanza.
Wakicheza nyumbani jijini Nouakchott, Mauritania walipata ushindi wa mabao 2-1 na kujikatia tiketi hiyo na kuongoza kundi lao kwa alama 12 .
Mabingwa zamani Zambia, walishindwa kufuzu baada ya kufungwa ugenini na Msumbuji, bao 1-0.
Ghana nao wajiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia jijini Addis, mabao yaliyofungwa na Jordan Ayew.
Ushindi huo unaiweka Black Stars katika nafasi ya pili katika kundi hilo kwa alama 6, nyuma ya Kenya ambayo ina alama 7.
Kenya na Ghana zina nafasi ya kufuzu baada ya Sierra Leon kufungiwa na FIFA.
Burundi inahitaji alama moja tu, katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Gabon jijini Bujumbura mwezi Machi mwaka 2019.
Tanzania ilihitaji kushinda mechi yake dhidi ya Lesotho, ili kufuzu katika michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39, lakini ilifungwa na Lesotho bao 1-0 mjini Maseru, na kudidimiza matumaini yake.
Timu zote zina alama tano, katika kundi L, na inahitaji kushinda mechi ya mwisho dhidi ya Uganda jijini Dar es salaam, na kuomba kuwa Cape Verde iishinda Lesotho ili kufuzu.
DRC ilitoka sare ya bao 1-1 na Congo, inahitaji ushindi dhidi la Liberia katika mechi ya mwisho, ili kufuzu.
Kundi la G, linaongozwa na Zimbabwe kwa alama nane, Liberia alama saba, DRC alama sita na Congo alama tano.
Kwa mara ya kwanza, michuano ya AFCON mwaka 2019 itakuwa na timu 24.