Na Fadhili Omary Sizya,
Ligi kuu Tanzania bara (TPL) inarejea wikiendi hii na leo hii itakuwa ni patashika uwanja wa Namfua Singida, wenyeji Singida United wanaikaribisha Mbao Fc.
Singida United
Walianza ligi kwa kufungwa 1-0 dhidi ya Biashara United, mechi ya pili wakashinda 1-0 dhidi ya Mwadui hii ni mechi ya tatu wanacheza mfululizo uwanjani kwao.
Klabu hiyo imeathirika kwa baadhi ya wachezaji muhimu kuuzwa katika dirisha lililopita la usajili ambapo Mudathir Yahya alimaliza mkataba wa mkopo na kurejea tena Azam Fc, Tafadzwa Kutinyu, Daniel Lyanga wameuzwa Azam na Deus Kaseke akiuzwa Yanga.
Kocha mkuu Hemedi Moroco atakuwa na kazi ya kukipanga kikosi chake kuikabili Mbao, eneo la ushambuliaji limemuangusha katika mechi za awali akimtegemea zaidi Hans Kwoffie mshambuliaji raia wa Ghana na Eliuter Mpepo ingizo jipya pia katika kikosi hicho ambao wote wameshindwa kuthibitisha ubora wao.
Wakicheza katika uwanja wao wa nyumbani huenda wakaibuka na ushindi haswa kutoka kwa hamasa ya mashabiki.
Mbao Fc
Msimu wa kwanza wakiwa na kocha mpya Amri Said “Stam” aliyechukua mikoba ya kocha Etienne Ndayiragije klabu hiyo imeshinda mechi zote 2 za awali ligi kuu Tpl.
Mbao imebadilika mno, msimu huu ikinunua baadhi ya wachezaji na kuongeza nguvu kikosi chao, ujio wa Pastory Athanas na Emmanuel Mtumbuka umeongeza kasi eneo la ushambuliaji.
Hii ni mechi yao ya kwanza msimu huu kucheza nje ya uwanja wa Ccm Kirumba kwahiyo ni kipimo sahihi kuthibisha uimara wao baada ya msimu wa 2017/2018 kuonekana kupoteza kiwango chao.