Mshambuliaji wa klabu ya soka ya Gor Mahia nchini Kenya, Meddie Kagere ni miongoni mwa wachezaji watano ambao wamekubaliwa rasmi kuwa raia wa Rwanda.
Hatua hii imekuja baada ya wachezaji zaidi ya 60 mwaka 2015 kupoteza uraia wao wa Rwanda wakati, nchi hiyo ilipoondolewa katika mashindano ya kufuzu kucheza fainali ya mataifa bingwa barani Afrika.
Hilo lilibainika baada ya Rwanda kumtumia mchezaji Dadi Birori ambaye alikuwa na ana pasi ya kusafiria ya DRC na kujiita Etekiama Tady Atigy.
Baada ya uamuzi huo wa CAF, Shirikisho la soka FERWAFA ilifanya maamuzi kuwa wachezaji pekee waliozaliwa nchini humo ndio watakaoichezea Amavubi Stars.
“Nimefurahi sana, kupata cheti hiki cha uraia, bidii niliyofanya imenisaidia, sasa nitakuwa huru kuichezea timu ya taifa,” amesema Kagere.
Kagere anaungana na wachezaji wengine kama Hussein Cyiza (Mukura), Jimmy Mashingirwa ‘Mbaraga’ Kibengo (AS Kigali), Andre Fils Lomami (Kiyovu) na Peter ‘Kagabo’ Otema (Musanze) ambao sasa watakuwa wanaichezea timu ya taifa.
Kagere ni mzaliwa wa Uganda lakini wazazi wake ni Wanyarwanda.