Shirikisho la Soka Tanzania TFF, jana lilimtangaza Mnigeria, Emmanuel Amunike kuwa kocha mpya wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, akichukua mikoba ya Salum Mayanga.Amesaini mkataba wa miaka miwili.
Kibarua cha kwanza cha Amunike itakuwa kuiongoza Tanzania katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika dhidi ya Uganda, mwezi ujao.
Anakuwa mwalimu wa pili kutoka Nigeria kufundisha soka Afrika Mashariki katika ngazi ya timu za taifa, Christian Chukwu aliifundisha Timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars kutoka mwaka 1998 hadi 2003.
Mbali na majukumu ya kuinoa Stars, Amunike pia amekabidhiwa majukumu ya kuzinoa timu za vijana chini ya miaka 23, 20 na 17.
Amunuke ni nani?
Alizaliwa mwaka 1970 katika Mji wa Eziobodo nchini Nigeria
Alianza soka la ushindani mwaka 1990 kwa kuichezea timu ya Concord na Julius Berger zote za Nigeria.
Mwaka 1991 hadi 1994 aliitumikia Zamalek ya Misri kabla kujiunga na Sporting Lisbon ya Ureno kutoka mwaka 1994 hadi 1996.
Amunike pia aliitumikia Barcelona ya Hispania kutoka mwaka 1996 hadi mwaka 2000.
Klabu nyingine alizowahi kuzitumikia enzi za uchezaji wake ni Albacete ya Hispania,Busan I’cons na Al-Wehdat.
Amunike pia aliitumikia timu ya Taifa ya Nigeria kwa miaka minane, na alikuwemo kwenye kikosi kilichoshiriki fainali za Kombe la dunia mwaka 1994 nchini Marekani.
Historia yake katika ufundishaji soka inabainisha kuanza miama kumi iliyopita ambapo amezinoa klabu mbalimbali zikiwemo Julius Berger, Al Hazm,Ocean Boys,Timu ya Vijana ya Nigeria chini ya miaka 17 na Klabu ya Al-Khartoum y Sudan.