Shirikisho la soka nchini Kenya FKF limemtangaza Mfaransa Sebastian Migne kuwa kocha mpya wa timu ya taifa Harambee Stars.
Migne anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mbelgiji Paul Put aliyejizulu mwezi Februari, miezi mitatu tu baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo.
Raia huyo wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 45, kabla ya kuteuliwa kuifunza Harambee Stars, alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Congo-Brazaville.
Kibarua chake cha kwanza kitakuwa ni kuisadia Kenya kufuzu katika michuano ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon.
Mara ya mwisho kwa Harambee Stars kufuzu katika michuano hiyo mikubwa ya Afrika ilikuwa ni miaka 14 iliyopita nchini Tunisia.
Mbali na Congo Brazaville, Migne amewahi pia kuifunza timu ya taifa ya DRC ya vijana wasiozidi miaka 20 mwaka 2013.
Kocha huyo, anaichukua Kenya ambayo inaorodheshwa kaika nafasi 113 kati ya 211 duniani.
Makocha zaidi ya 10 walikuwa wameomba kazi ya kuifunza Kenya.