Michuano ya tano hatua ya makundi, kuwania taji la klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika inachezwa mwishoni mwa juma hili, kuanzia siku ya Ijumaa.
Leo, klabu ya Al-Ahly ya Misri itakuwa wenyeji wa ZESCO United kutoka Zambia katika mchuano muhimu wa klabu bingwa.
Mchuano huo utachezwa katika uwanja wa El Arba mjini Alexandria kuanzia saa tatu usiku saa za Afrika Mashariki.
ZESCO United inakwenda katika mchuano huu ikiwa ya pili katika kundi la A kwa alama 7 sawa na Wydad Casablanca huku Al-Ahly ikiwa ya mwisho kwa alama 4 baada ya kushinda mechi 1 kati ya nne ilizocheza.
Mchuano mwingine katika kundi hili ni kati ya Wydad Casablanca ya Morroco dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast, mchuano utakaochezwa siku ya Jumapili katika uwanja wa Prince Moulay Abdellah mjini Rabat.
Mchuano wa kundi B, Zamalek ya Misri itakuwa mwenyeji wa Enyimba ya Nigeria, siku ya Jumapili katika uwanja wa Petro Sport jijini Cairo.
Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayo inaongoza kundi hili kwa alama 9 itamenyana na Enyimba ugenini katika uwanja wa Adokiye Amiesimaka mjini Port Hartcourt.
Klabu ya Yanga FC kutoka Tanzania, siku ya Jumamosi itacheza mchuano wake wa tano kujaribu kupata ushindi, baada ya kusindwa katika mechi nne zilizopita.
Vijana hao wa Jangwani kutoka jijini Dar es salaam watakuwa katika uwanja wa Taifa kuwakabili MO Bejaia ya Algeria.
Mchuano wa kwanza kati ya timu hizi mbili, MO Bejaia iliishinda Yanga bao 1 kwa 0 ugenini mwezi Juni mjini Bejaia.
Matumaini ya Yanga FC kufuzu katika hatua ya nusu fainali yamedidimia hadi sasa kwa sababu ni wa mwisho katika kundi hili kwa alama 1.
Viongozi wa kundi hili, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wana alama 10, baada ya kushinda mechi tatu na kutoka sare mechi moja.
Siku ya Jumapili Mazembe watakuwa ugenini kumenyana na Medeama ya Ghana.
Mechi za kundi la B, zinachezwa leo, Al-Ahli Tripoli ya Libya itachuana na FUS Rabat ya Morocco huku Etoile du Sahel ya Tunisia na Kawkab Marrakech ya Morocco.