Michuano ya soka, mzunguko wa pili kutafuta nafasi ya kufuzu kucheza katika hatua ya kwanza kuwania taji la Shirikisho na klabu bingwa barani Afrika, itachezwa siku ya Jumanne na Jumatano wiki hii.
APR ya Rwanda iliyoanza vizuri nyumbani katika michuano ya Shirikisho, kwa kupata ushindi wa mabao 4-0, itakuwa ugenini kucheza na Anse Reunion ya Ushelisheli.
Gendarmerie Nationale FC ya Djibouti nayo itakuwa mwenyeji wa Simba SC ya Tanzania mjini Djibouti.
Simba, wanaofahamika kwa jina maarufu kama wekundu wa Msimbazi, wanakwenda katika mchuano huo wa marudiano wakiwa na ushindi mkubwa wa mabao 4-0.
Siku ya Jumatano, itakuwa ni zamu ya Zimamoto ya Zanzibar, kupata ushindi dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia, ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele.
Mchuano wa kwanza, uliochezwa Visiwa Zanzibar, timu zote mbili zilitoka sare ya bao 1-1, matokeo ambayo yanaipa kazi kubwa Zimamoto wakiwa ugenini.
Fosa Juniors ya Madagascar, itakuwa wenyeji wa AFC Leopards ya Kenya.
Mchuano wa kwanza, ulichezwa katika uwanja wa Bukhungu katika Kaunti ya Kakamega, na timu zote mbili kutoka sare ya bao 1-1.
AFC inahitaji kupata bao ugenini ili, kufuta bao walilofungwa nyumbani.
Ratiba nyingine:-
Olympique Star (Burundi) v Etoile Filante (Burkina Faso) 0-0
AS Maniema Union (DRC) v AS Mangasport (Gabon) 1-0
Timu ambazo tayari zimefuzu katika hatua ya kwanza ni pamoja na SuperSport United (Afrika Kusini), Enyimba (Nigeria), DC Motema Pembe (DRC), Nkana (Zambia), Zamalek (Misri), Nkana (Zambia).
Hali itakuwa hivyo katika michuano ya klabu bingwa hasa kwa timu za Afrika Mashariki na Katii.
Baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 ikiwa ugenini CnaPS Sport ya Madagascar, itakuwa ugenini kumenyana na KCCA ya Uganda jijini Kampala siku ya Jumatano.
Leones Vegetarianos ya Equatorial Guinea itakuwa wenyeji wa Gor Mahia ya Kenya, baada ya kufungwa mabao 2-0.
Saint Loius Suns United ya Ushelisheli itakuwa nyumbani kumenyana na Young Africans au Yanga ya Tanzania, baada ya kufungwa bao 1-0 wakiwa ugenini.
Ratiba:-
LLB Academic FC (Burundi) v Rayon Sport (Rwanda) 1-1
ZESCO United (Zambia) v JKU (Zanzibar) 0-0