Connect with us

 

Michuano ya soka hatua ya nusu fainali kuwania taji la klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika inachezwa mwishoni mwa wiki hii katika viwanja mbalimbali barani Afrika.

Zamalek ya Misri inashuka dimbani nyumbani siku ya Ijumaa usiku kumenyana na Wydad Casablanca ya Morroco vlabu, vyote kutoka Kaskazini mwa Afrika, katika mchuano wa kwanza kuwania taji la klabu bingwa.

Siku ya Jumamosi, pambano la vlabu ya Kusini mwa Afrika vitapambana.

ZESCO United ya Zambia itakuwa wenyeji wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mchuano utakaochezwa katika uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola.

Mara ya mwisho vlabu ya Kusini mwa Afrika kumenyana katika hatua hii ya nusu fainali katika michuano hii, ilikuwa ni miaka 15 iliyopita wakati Mamelodi Sundowns ilipochuana na Petro Atletico ya Angola.

Michuano hii inachezwa nyumbani na ugenini na hatua ya marudiano itachezwa siku ya Jumamosi ijayo tarehe 24 mwezi huu wa Septemba.

Mambo muhimu ya kufahamu katika historia ya michezo hii:-

Mabao 461 yamefungwa katika michuano 187 iliyochezwa katika michuano hii tangu mwaka 1964.

Vlabu vingi vinapenda kuanzia ugenini na takwimu zinaonesha kuwa kumekuwa na ushindi mara 55 kati ya michuano 90 ambazo zimeanza kuchezwa ugenini.

Mwaka 1976, klabu ya Hafia kutoka Guinea iliyokuwa imefungwa katika mchuano wa kwanza mabao 3-0 dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast, iliweka historia kwa kufanikiwa kupata ushindi wa mabao 5-0 nyumbani jijini Conankry katika mchano wa marudiano.

Idadi kubwa ya michuano ya hatua ya nusu fainali huishia kwa sare na baadaye kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti.

Mbali na michuano ya klabu bingwa, michuano ya Shrikisho nayo inapigwa.

TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itaanzia ugenini, kumenyana na mabingwa watetezi Etoile du Sahel ya Tunisia siku ya Jumamosi katika uwanja wa Olympique de Sousse, mjini Sousse.

Mazembe ambao wanashiriki katika michuano hii baada ya kuondolewa katika michuano ya kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika, waliloshinda msimu uliopita, sasa wanalenga kushinda taji hili ili kuwarejea imani mashabiki wake.

Klabu hii yenye makao yake mjini Lubumbashi Kusini Mashariki mwa DRC, imeshiriki mara nne katika historia ya michuano hii na mwaka 2013 ilifika katika hatua ya fainali.

Siku ya Jumapili, MO Bejaia nayo itakuwa nyumbani kumenyana na FUS Rabat katika mchuano mwingine wa timu kutoka Kaskazini mwa Afrika.

Mambo muhimu kuhusu michuano hii ya Shirikisho:-

Kumekuwa na michuano 28 ya nusu fainali ya taji hili la Shirikisho tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009.

Kumekuwa na ushindi mara 16 kwa vlabu vinavyoanza kucheza nyumbani, sare sita lakini ushindi mara sita umepatikana ugenini.

Vlabu vingi vimeonekana kupenda kuanza kucheza ugenini na historia inaonesha kuwa vlabu 14 vimepata ushindi baada ya kuanza kucheza ugenini.

Mara nyingi, michuano ya nusu fainali humalizika kwa ushindi wa 1-0 mechi 11, ikifuatwa na ushindi wa 2-1 mara tano na 0-0 mara nne.

More in