Misri imejiondoa kushiriki katika michuano ya soka katika mashindano ya Afrika yatakayofanyika mwezi ujao wa Septemba nchini Congo Brazaville.
Shirikisho la soka barani Afrika CAF limethibitisha hatua hiyo ya Misri bila ya kutoa ufafanuzi wowote.
Hata hivyo, vyombo vya habari jijini Cairo vimekuwa vikiripoti kuwa kocha wa timu ya taifa Hossam El Badry anasema kikosi chake ni dhaifu.
Sheria za mashindano haya zinawaruhusu tu wachezaji wasiozidi miaka 23 kushiriki na miongoni mwa wachezaji shupavu wa Misri akiwemo kiungo wa kati Kahraba hatakuwepo wakati wa michuano hiyo.
Misri ilifuzu katika michuano hiyo baada ya kuishinda Kenya na Burundi katika hatua ya kufuzu.
Kuondoka kwa mabingwa mara mbili wa michuano hiyo kuna maana kuwa kundi lao linasalia na timu tatu Ghana, Nigeria na Senegal huku Burundi ikikataa kuziba pengo la Misri.
Michuano hiyo itafungua milango yake kati ya tarehe 6 hadi 18 mwezi Septemba na mataifa mengine yanayoshiriki ni pamoja na wenyeji Congo Brazzaville, Sudan, Zimbabwe na Burkina Faso.