Mambo mengi kuhusu maendeleo ya soka yatajadiliwa katika mkutano huo ikiwemo kuagalia hali ya usimamizi wa soka katika mataifa kadhaa barani Afrika.
Mwezi Agosti, FIFA ilikuwa imetishia kuifungia Nigeria kutoshiriki katika masuala ya soka iwapo serikali ingeendelea kuingilia usimamizi wa mchezo wa soka nchini humo na kumuunga mkono Chris Giwa, aliyeonekana kuungwa mkono na serikali kumwondoa madarakani Pinnick Amaju rais wa NFF.
Hata hivyo, maendeleo yaliyotokea nchini Nigeria baada ya kuchaguliwa tena kwa Pinnick kuongoza NFF, ni suala ambalo litajadiliwa jijini Kigali.
Hili lilionekana kukosa nguvu baada ya kufanyika kwa Uchaguzi katika Shirikisho la soka nchini humo NFF, na Amaju Pinnick akachaguliwa tena.
Onyo kama hilo pia lilitolewa nchini Ghana, baada ya serikali kuamua kuingilia mchakato wa kumchunguza aliyekuwa rais wa Shirikisho la soka nchini humo Kwesi Nyantakyi anayedaiwa kuhusika na ulaji rushwa.
Hata hivyo, baada ya tahadhari hiyo, serikali ya Ghana iliamua kuacha uchunguzi huo na kuiachia FIFA kuendeleza uchunguzi wake.
Aidha, uongozi huo wa juu wa FIFA, utajadili hatua iliyoichukulia Sierra Leone , baada ya serikali nchini humo kuvamia Ofisi za soka jijini Freetown na kumlazimisha rais wa soka nchini humo Isha Johansen kujiuzulu kwa madai ya ufisadi.
Uamuzi huu unamaanisha kuwa, Sierra Leone haiwezi kushiriki katika michuano ya kimataifa hasa yale ya kufuzu kucheza fainali ya bara Afrika nchini Cameroon mwaka ujao.
Hatua hii ya FUFA imeipa Kenya nafasi kubwa ya kufuzu kucheza fainali ya bara Afrika, iwapo kifungo hicho kitaendelea kuwepo.