Kama ilivyotarajiwa na wapenzi na mashabiki wa klabu ya Simba, ndivyo ilivyotokea leo baada ya mfanyabiashara mashuhuri nchini Tanzania Mohammed Dewji kushinda zabuni ya kuwekeza kwenye klabu hiyo.
Dewji ni mwanachama pekee aliyejitokeza kuomba kununua asilimia 50 za hisa za klabu hiyo kwa fedha zinazokadiliwa kufikia bilioni 20 za Tanzania.
Mwenyekiti wa kumtafuta mwekezaji wa Simba Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ametangaza Dewji kushinda zabuni hiyo katika mkutano wa wanachama wa Simba uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu julius Nyerere uliopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Baada ya tangazo hilo mashabiki wa Simba wamemiminika kwenye mitandao ya kijamii kushangilia hatua hiyo wakidai italeta mafaniko kwa klabu hiyo.
Kwa hatua hiyo sasa Dewji atamiliki asilimia 50 ya hisa huku nyingine 50 zikimilikiwa na wanachama wa Simba.
Hatua hiyo ni mageuzi ya kwanza katika soka la Tanzania hususani kwa klabu za Simba na Yanga ambazo kwa zaidi ya miaka 80 ya uhai wake zimekuwa zikiendeshwa kwa michango ya wanachama.
Kabla ya kuonesha nia yake Dewji aliahidi ikiwa atafanikiwa kushinda zabuni hiyo atafanikisha mchakato wa Simba kuwa na uwanja wake na vitega uchumi vingine ambavyo vitainufaisha klabu hiyo na kuiwezesha kushindana na klabu kubwa barani Afrika zikiwemo TP Mazembe, Enyimba, Supersports na National Al Ahly.
Aidha Dewji aliahidi kufanikisha usajili wa wachezaji mahiri kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
Kwa mujibu wa jarida la Forbes hadi kufikia mwaka 2015 Dewji mwenye umri wa miaka 42 ana utajiri unaokisiwa kufikia dola za Marekani bilioni 1.1