Shirikisho la soka barani Afrika, limetangaza kuwa Morocco ndio itakayokuwa mwenyeji wa michuano ya bara Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani CHAN.
Uamuzi wa huu umefikiwa baada ya mkutano wa viongozi wa soka barani Afrika waliokutana kwa dharura mjini Lagos, nchini Nigeria Jumamosi usiku.
Equatorial Guinea ilikuwa imeomba nafasi hiyo lakini haikufanikiwa. Ethiopia nayo haikufika mbili bora baada ya kukosa barua kutoka serikalini kutoa hakikisho la kufanikisha michuano hiyo.
Morocco imechukua nafasi ya Kenya ambayo, ilipokonywa haki ya kuandaa fainali hii kwa sababu ya maandalizi mabaya kuelekea fainali ya CHAN mwezi Januari.
Hii ni nafasi ya kipekee kwa Morocco ambayo haijawahi kuwa mwenyeji wa michuano mikubwa ya soka barani Afrika, tangu mwaka 1988 ilipoandaa michuano ya mataifa bingwa barani Afrika.
Mwaka 2015, Morocco ilipewa nafasi ya kuandaa tena fainali ya AFCON lakini ikajiondoa kwa hofu ya maambukuzi ya Ebola.