Nigeria na Afrika Kusini, zitamenyana kuanzia saa moja jioni, saa za Afrika Mashariki katika fainali ya kuwania taji la bara Afrika kwa upande wa wanawake.
Mechi inachezwa katika uwanja wa Kimataifa wa Accra jijini Ghana.
Mwamuzi wa mchuano huu ni Gladys Lengwe kutoka Zambia.
Nigeria, ambao ni mabingwa watetezi, walifuzu katika hatua ya fainali baada ya kuishinda Cameroon kwa mabao 4-2, katika mechi ya nusu fainali, huku Afrika Kusini wakiishinda Mali mabao 2-0.
Siku ya Ijumaa, Cameroon iliishinda Mali mabao 4-2 katika mechi muhimu ya kumtafuta mshindi wa tatu.
Mataifa mengine yaliyoshiriki ni pamoja na wenyeji Ghana, Algeria na Equitorial Guinea.
Nigeria imeshinda taji hili mara 10, mwisho ilikuwa ni mwaka 2016. Afrika Kusini haijawahi kushinda taji hili lakini imefika hatua ya fainali mara nne, mwaka 1995, 2000, 2008 na 2012.
Nigeria, Cameroon na Afrika Kusini, zimefuzu kucheza katika fainali za kobe la dunia mwaka 2019 jijini Paris nchini Ufaransa.