Michuano ya soka kutafuta ubingwa wa Afrika kwa upande wa wanawake, inaendelea siku ya Jumanne na Jumatano nchini Cameroon.
Wenyeji Cameroon walioanza vizuri mwishoni mwa wiki iliyopita, wanacheza mchuano wake wa pili dhidi ya Afrika Kusini lakini Zimbabwe na Misri watamenyana pia kutafuta ushindi wa kwanza katika michuano hii.
Siku ya Jumatano katika michuano ya kundi B, watani wa jadi kutoka Afrika Magharibi, Nigeria ambao ni mabingwa watetezi, watamenyana na Ghana huku Kenya iliyoanza vibaya ikimenyana na Mali.
Mbali na michuano hiyo inayoendelea, Super Falcons ya Nigeria na Banyana Banyana ya Afrika Kusini ina makocha wa kike, lakini mataifa mengine yote yanafunza na makocha wa kiume.
Mfahamu kocha Florence Omagbemi
Ana umri wa miaka 41.
Kocha wa Nigeria tangu mwaka 2.016, baada ya kuchukua nafasi ya Christopher Danjuma baada ya matokeo mabaya katika michuano ya Afrika mwaka 2015.
Mchezaji wa zamani wa Nigeria tangu mwaka 1991 na kuisaidia nchi yake kushinda mataji manne ya Afrika, akiwa nahodha mwaka 1998,2000,2002 na 2004.
Kabla ya kuwa kocha wa Super Falcons, aliwahi kuwa naibu kocha wa kikosi cha wachezaji wenye chini ya umri wa miaka 20.
Mfahamu kocha Desiree Ellis
Umri wa miaka 53.
Mchezaji wa zamani na nahodha wa timu ya taifa kati ya mwaka 1993-2002.
Aliteuliwa kuwa kocha baada ya kuondoka kwa kocha wa zamani Vera Pauw raia wa Uholanzi.
Kabla ya kupata nafasi hii alikuwa naibu wa Vera kwa muda wa miaka mwili na nusu iliyopita.