Connect with us

 

Nigeria imetetea taji la soka kwa wanawake kwa mataifa ya Afrika baada ya kuifunga Cameroon bao 1-0 katika fainali iliyochezwa jijini Yaounde siku ya Jumamosi jioni.

Wenyeji Cameroon waliutawala mchezo huo mbele ya maelfu ya mashabiki wa nyumbani waliofurika katika uwanja wa Ahmadou Ahidjo akiwemo rais Paul Biya.

Bao la Nigeria lilitiwa kimyani na Desire Oparanozie katika dakika 10 za mwisho wa mchuano huo ulionekana kuisha sare ya kutofungana.

Bao hilo la lala salama, lilionekana kuwavunja moyo wachezaji wa Cameroon huku juhudi zao za kusawazisha zikiambulia patupu baada ya mwamuzi wa mchuano huo Aissata Ameyo Amegee kutoka Togo kupuliza kipenga cha mwisho.

Ilikuwa ni fainali ya nne kati ya mataifa haya mawili baada kukutana mwaka 1991, 2004 na 2014 lakini katika michuano hiyo yote, Nigeria iliibuka mabingwa.

Hili ni taji la nane la Nigeria katika michuano hii na inaendelea kuweka historia ya kuwa taifa bora katika michuano hii.

Ghana iliishinda Afrika Kusini bao 1-0 siku ya Ijumaa na kumaliza katika nafasi ya tatu.

Michuano ya mwaka 2018 itachezwa nchini Ghana.

More in AWCON