Wakati timu ya Taifa ya Tanzania Bara Kilimanjaro Stars kesho ikitarajiwa kuanza kampeni ya kuwania taji la michua o ya Kombe la Chalenji kwa kuvaana na Libya, wachezaji wa zamani wa timu hiyo wamesema ina nafasi ya kufika mbali.
Tanzania Bara imepangwa kundi A sambamba na wenyeji Kenya, Zanzibar, Libya na Rwanda.
Beki wa zamani wa timu hiyo Stephano Mwasika amesema ikiwa wachezaji watajitambua na kutambua wajibu wao kwa nchi wanaweza kufanya viziuri na kuwatoa tongotongo mashabiki wa soka ambao kwa muda mrefu hawajaonja mafanikio ya timu hiyo.
“Mashindano si rahisi, timu za Kundi A zote zina uwezo na wachezaji wa kanda hii wanafahamiana. Lazime kuwe na mkakati wa kusaka ushindi kila mchezo,”alisema Mwasika ambaye alikuwemo kwenye kikosi cha timu hiyo kilichoshinda taji mwaka 2010 kwenye mashindano yaliyofanyika Dar es salaam.
Kiungo wa zamani wa Simba na Kilinjaro Stars, Mohammed Banka amesema Kilimanjaro Stars lazima ijidhatiti na kufanikiwa kushinda mechi za hatua ya makundi ili isonge mbele.
“Kenya wako nyumbani na wana faida hiyo, pia Rwanda na Zanzibar nazo ziko vizuri. Muhimu wachezaji wafuate maelezo ya kocha na kujituma kwenye kila mchezo watakaocheza, wanaweza kufanikiwa,”amesema Banka ambaye pia aliwahi kuitumikia timu ya Taifa ‘Taifa Stars’