Rais wa Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA Michel Platini ambaye amesimamishwa uanachama wa Kamati ya utendaji ya Shirikisho la soka duniani FIFA kwa siku tisini kwa tuhma za ufisadi, amekiri kuwa hakuna stakabadhi yoyote inaonesha alipokea fedha kutoka kwa uongozi wa FIFA.
Platini ambaye alipokea Dolla Milioni 2 kama malipo ya kumshauri Sepp Blatter ambaye pia amesimamishwa kazi, ameliambia Gazeti la Ufaransa la kila siku Le Monde, malipo aliyopewa yalikuwa ni makubaliano binafsi na Blatter. Raia huyo wa Ufaransa ambaye alikuwa na ndoto za kuwa rais wa FIFA, amedai Blatter amekuwa na njama za kummaliza kisiasa. Blatter alipozungumza juma lilolipa, alisisitiza kuwa hana kosa lolote kwa kumlipa Platini na kuongeza kuwa yalikuwa makubaliano kati yao. Kamati ya maadili iliwasimamisha kazi Blatter na Platini juma moja lililopita, kwa tuhma za ufisadi katika Shirikisho hilo. Nchini Ujerumani, viongozi wa mashtaka wanasema wanachunguza madai kuwa viongozi wa soka nchini humo walitoa rushwa kwa maafisa wakuu wa FIFA ili kupata nafasi ya kuwa wenyeji wa kombe la dunia mwaka 2006. Maafisa wakuu wa FIFA wameendelea kushtumiwa kuhusika na ulaji rushwa na uchaguzi mpya wa kumpata rais mwingine umeratibiwa kufanyika tarehe 26 mwezi Februari mwaka 2016.