Timu ya Tanzania Prisons imeanza maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC.
Timu hizo zitavaana katika mchezo unaotabiriwa kuwa na ushindani mkali utakaofanyika Novemba 18 kwenye Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya, Kusini Magharibi mwa Tanzania.
Kocha wa Prisons Abdallah Mohammed amesema Simba ni timu kubwa na hawana budi kujipanga kikamilifu ikiwa wanataka kushinda mchezo huo.
“Ni mechi muhimu kwetu na mashabiki wetu, tunajua Simba watakuja wakihitaji matokeo lakini na sisi tumeanza maandalizi mapema,”alisema Mohammed.
Simba imekuwa ikipata wakati mgumu inapokutana na Prisons hususani kwenye Uwanja wa Sokoine.
Naye beki wa Prisons Salum Kimenya amesema wanachohitaji kwenye mchezo huo ni pointi tatu ili kuendelea kujiweka mahala pazuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Simna inaongoza Ligi ikiwa na alama 19 baada ya kucheza mechi tisa wakati Tnaznia Prisons inashika nafasi ya tano ikiwa na alama 14.