Rais wa Tanzania John Magufuli, amewaambia wachezaji wa timu ya taifa ya soka Taifa Stars, hafurahishwi na matokeo ya timu hiyo hasa katika kampeni ya kufuzu kucheza fainali ya mashindano ya bara Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon.
Magufuli amekutana na wachezaji wa timu ya taifa katika Ikulu jijini Dar es salaam ,baada ya ushindi dhidi ya Cape Verde katika mchuano muhimu wa hatua ya makundi wiki hii.
“Napenda sana michezo, lakini mimi sio shabiki wa timu yoyote hapa Tanzania,” alisema rais Magufuli.
“Sipendi kushindwa, na ni aibu sana watu Milioni 55 kushindwa kupata kombe la Afrika, “ aliongeza.
Hata hivyo, Magufuli amesema ameanza kupata matumaini baada ya ushindi wa nyumbani na kuahidi kuwapa Shilingi za nchi hiyo Milioni Elfu Hamsini, kufanikisha maandalizi yao.
“Mlipofungwa mabao 3 nilikata tamaa, na mlipofunga mabao mawili, sikufurahi kwa sababu mnadaiwa moja,” alisema.
“Bado hamjashinda, bado,” alisisitiza.
Aidha, amewashtumu viongozi wa zamani wa soka aliosema waliotumia vibaya fedha zilizotumwa na Shirikisho la soka kusaidia maendeleo na soka nchini humo.
“Kupotea kwa fedha, ni suala ambalo linawakatisha tamaa wachezaji hata ndani ya klabu za soka,”
Taifa Stars, ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde wiki hii, na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu katika michuano hiyo.
Tanzania ni ya pili katika kundi L, ikiwa na alama tano baada ya kushinda mechi moja na kutoka sare michuano miwili. Kundi hili linaongozwa na Uganda ambayo ina alama 10.
Kufuzu katika fainali hizo, Tanzania inahitaji kushinda mechi ijayo dhidi ya Lesotho jijini Maseru, ikisubiri mechi ya mwisho mwezi Machi mwaka 2019.
Mara ya mwisho kwa Tanzania kufuzu katika fainali ya Afrika ilikuwa ni mwaka 1980 nchini Nigeria.