Mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC kesho wanatarajiwa kukabidhiwa ubingwa wao katika hafla itakayofanyika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo anatarajiwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dr. John Magufuli.
Simba imeshinda ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kupita miaka mitano, ikiwa na alama 68 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote inayoshiriki ligi hiyo.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF, Wallace Karia aliwaambia waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam mapema wiki hii kwamba TFF iliamua kumualika Rais Magufuli ili pia alipokee kombe la Cecafa ambalo timu yavijana chini ya miaka 17 ilitwaa nchini Burundi.
“Uongozi wetu unatimiza mwaka mmoja na tumeona tumualike mheshimiwa rais na tunashukuru kwa kuwa ombi letu limefanyiwa kazi kupitia wizara ya habari utamaduni na michezo, tunamshukuru sana Mheshimi wa Rais ,”alisema Rais Karia.
Kutokana na matukio hayo kufungana, mchezo baina ya Simba na Kagera Sugar utaanza saa nane mchana ili kutoa nafasi kwa rasi Magufuli kukabidhi kombe kwa Simba na kupokea kombe la Cecafa.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba Haji Manara amesema klabu yake imefurahishwa na hatua ya rais kukubali mwaliko huo.
“Simba tumejiandaa kutoa burudani ya kutosha tunawaomba mashabimki wa jklabu ya Simba wanunue jezi za ubingwa na kujitokeza kwa wingi uwanjani,.”amesem Manara.
Kiingilia cha chini katika mchezo huo kitakuwa shilingi 2000 sawa na dola moja ya marekani.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Rais wa Tanzania, Dr.John Magufuli kushiriki tukio la Michezo akiwa uwanjani tangu alipochaguliwa kuwa rais wa Tanzania, Oktoba 2015.