Rais wa Shirikisho la soka nchini Uganda Moses Magogo anataka kujiuzulu kwa rais wa Baraza la soka Afrika Mashariki na Kati CECAFA, Mutasim Gafaar ajiuzulu.
Magogo amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Baraza hilo Nicholas Musonye na kulalamika kuwa Mutasim raia wa Sudan, hana muda wa kushughulikia masuala ya soka katika ukanda wa CECAFA kama kiongozi.
Aidha,ameongeza kuwa Mutasim amekosa mwelekeo wa kusaidia kuinua soka Afrika Mashariki na Kati.
Rais Magogo ambaye anaonekana kuchoshwa na uongozi wa Mutasim, amekuwa akisusia mikutano ya Kamati kuu ya CECAFA na kumtuma naibu wake Justus Mugisha.
Barua hii imekuja wiki moja baada ya kufanyika kwa Uchaguzi wa viongozi wa soka nchini Sudan na aliyekuwa Mwanakamati katika Shirikisho la soka barani Afrika CAF, Kamal Shaddad, kuchaguliwa kumrithi Mutasim ambaye amekuwa rais wa soka nchini humo kwa muda mrefu.