Na Victor Abuso,
Rais wa ligi kuu ya soka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (LINAFOO) Simon Kayoyo Umbela amejiuzulu.
Umbela amesema amechukua hatua hii na kuwasilisha barua yake kwa viongozi wa Shirikisho la soka nchini humo baada ya kutofautiana nao kuhusu ratiba ya ligi kuu ya taifa.
“Nilitembelea Ofisi ya Shirikisho la soka hivi leo, na nimewaambia naacha kazi na sasa ni wao kuamua ikiwa watanishukuru au la,” alisema.
Mbali na mgogoro huo, Umbela amesema kuwa amechukua uamuzi huo kwa sababu za kibinafsi.
Mvutano kuhusu ni lini ligi kuu inastahili kufika tamati na kurejelewa umeivutia pia serikali ambayo imependekeza kuwa ligi hiyo lazima ifikie mwisho ifikapo tarehe 31 mwezi Mei kila mwaka.
Aidha, uongozi wa LINAFOOT, ulipendekeza kuongezwa kwa muda wa kumalizika kwa ligi hiyo kama ilivyokuwa imependekezwa na Shirikisho la soka FECOFA lakini tofauti zikashamiri kai ya pande hizo mbili.
Ikiwa mwafaka hautofikiwa haraka iwezekanavyo, itakuwa ni vigumu kuandaa taji la FECOFA kama ilivyozoeleka na klabu ya AC Vita Club itatawazwa mabingwa wa taji hilo, TP Mazembe itashika nafasi ya pili na Don Bosco nafasi ya tatu.
Nchini DRC mshindi wa kwanza na wa pili wa ligi kuu huwakilisha nchi hiyo katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika, huku mshindi wa tatu akifuzu katika michuano ya Shirikisho barani Afrika.