Mahakama nchini Nigeria inasema Rais wa shirikisho la soka nchini humo Amaju Pinnick pamoja na maafisa wengine wanne wa ngazi za juu katika shirikisho hilo wanakabiliwa na tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya Mamilioni ya dola kutoka kwa Shirikisho la soka duniani FIFA.
Kamati maalumu ya uchunguzi kuhusu matumizi ya mali za umma nchini humo, imeibua tuhuma dhidi Pinnick pamoja na makamu wake Seyi Akinwunmi na Shehu Dikko katibu mkuu wa shirikisho hilo.
Wengine wanaotuhumiwa ni pamoja na Sanusi Mohammed pamoja na mjumbe wa kamati ya Shirikisho hilo Ahmed Yusuf.
Tuhuma hizo zinahusisha hatua ya viongozi hao kushindwa kuthibitisha umiliki wa mali zao, na matumizi mabaya ya kiasi cha dola millioni 8.4 zilizotolewa na FIFA kwa ajili ya ushiriki wa Nigeria katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil.
Aidha viongozi hao wanataajiwa kufikishwa katika Mahakama ya juu ya shirikisho mjini Abuja ,ingawa tarehe ya kufikishwa Mahakamani hapo itatangazwa.