Tume ya kupambana na ufisadi nchini Nigeria imesema, itawafungulia kesi ya ufisadi, viongozi wakuu wa soka nchini humo.
Mkuu wa tume hiyo, Obono-Obla amesema tume hiyo ina ushahidi wa kutosha dhidi ya viongozi wa soka nchini humo wakiongozwa na rais wa NFF ambaye pia ni naibu raia wa Shrikisho la soka barani Afrika, Amaju Pinnick, na manaibu wake wawili, Seyi Akinwunmi na Shehu Dikko.
Masaibu yameanza kumsakama Bwana Pinnick ambaye mwezi Septemba mwaka 2018 kuchaguliwa kwa muhula wa pili kuongoza soka nchini humo baada ya kipindi cha mzozo wa usimamizi wa soka kati yake na Chris Giwa ambaye amekuwa akiungwa mkono na serikali.
Pinnick na wenzake, wanatuhumiwa kutumia fedha kutoka Shirikisho la soka duniani FIFA, ambazo ni Dola Milioni 9.5 kwa matumizi yao binafsi mwaka 2015.
Mbali na FIFA, serikali ya Nigeria imekuwa ikitoa fedha kusaidia kuendesha masuala ya soka nchini humo.
Hata hivyo, kanuni za FIFA haziruhusu serikali kuingilia masuala ya soka kwa nchi mwanachama.