Rufani iliyokatwa na klabu ya Yanga ikidai Mbeya City ilizidisha wachezaji katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa mwezi uliopita katika uwanja wa Sokoine imetupiliwa mbali.
Yanga ilikata rufaa ikipinga mchezaji Ramadhan malima wa Mbeya City kuingia uwanjani kushangilia bao la kusawazisha la Mbeya City licha ya kuwa alikuwa ametolewa nje kwa kadi nyekundu katika mchezo huo.
Mchezaji huyo amesimamishwa kwa mujibu wa kanuni ya 95 ya Ligi Kuu mpaka suala lake litakaposikilizwa na kamti ya nidhamu ya Ligi hiyo.
Yondani apigwa stop.
Katika hatua nyingine bodi inayosimamia Ligi Kuu Tanzania bara, imemsimamisha kucheza beki wa yanga Kelvin Yondan baada ya kubainika kumtemea mate mchezaji wa Simba, Asante Kwasi katika mchezo wa Ligi Kuu baina ya Simba na Yanga.
Yondan alimtemea mate Kwasi dakika ya 37 wakati wakigombea kucheza mpira wa faulo langoni mwa Yanga. Katika mechi hiyo Yanga ilipoteza kwa bao 1-0.
Adhabu ya kumsimamisha mchezaji huyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 9(5) inayosimamia Ligi hiyo na mpaka suala la mchezaji huyo litakaposikilizwa na kamati ya nidhamu.