Shirikisho la soka nchini Rwanda Ferwafa, limesema linamaliza mipango ya mwisho mwisho ya maandalizi ya kuomba nafasi ya kuandaa michuano ya duniani kwa vijana wasiozidi miaka 17, mwaka 2019.
Rais wa FERWAFA Vincent Nzamwita amesema nchi yake ina uwezo wa kuandaa fainali hiyo, ikiwa itapata nafasi hiyo.
“Tayari tumeiambia FIFA, nia yetu ya kuandaa kombe la dunia kwa vijana, na tayari tumewapa nyaraka zetu,” amesema.
Rwanda ina hadi Ijumaa, kuweka ombi lao rasmi kwa Shirikisho la soka duniani FIFA.
Ikiwa Rwanda itafanikiwa kuandaa michuano hii, itainua jina la nchi ya Rwanda, ukanda wa Afrika Mashariki na bara Afrika.
Ombi hili la Rwanda limekuja baada ya kufanikiwa kuandaa fainali ya CHAN mwaka uliopita.
Kombe la dunia la mwaka huu litafanyika nchini India kuanza tarehe 6 mwezi Oktoba.
Mataifa 24 yatashiriki huku Afrika ikiwakilishwa na Ghana, Guinea, Mali na Niger.