Mabingwa wa soka taji la klabu bingwa barani Afrika CAF, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesindwa kuendelea kusaka taji la dunia katika michuano ya vlabu inayoendelea nchini Japan.
Mazembe walifungwa na wenyeji Sanfrecce Hiroshima mabao 3 kwa 0 siku ya Jumapili jijini Osaka katika hatua ya mchuano wa robo fainali.
Mazembe waliofika katika hatua ya fainali ya michuano hii miaka mitano iliyopita, walioutawala mchuano huo wa robo fainali lakini wakashindwa kutumia nafasi nyingi walizopata kupata mabao.
Bao la kwanza la klabu ya Sanfrecce Hiroshima lilitiwa kimyani na Tsukasa Shiotani, baada ya mkwaju wa kona uliopigwa na Yusuke Chajima.
Bao la pili lilifungwa na beki Kazuhiko Chiba katika dakika ya 11 huku Takuma Asano aliyeingia kipindi cha pili akiipa klabu yake bao la tatu.
Mashambulizi ya wachezaji wa kulipwa kutoka Tanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu yaligonga mwamba kutokana na uimara wa beki ya wapinzani wao.
TP Mazembe sasa itachuana na Cub America ya Mexico siku ya Jumatano kutafuta mshindi wa nafasi ya tano katika mashindano hayo.
Mapema siku ya Jumapili, Club America ilipoteza katika hatua ya robo fainali baada ya kufungwa na Guangzhou Evergrande ya China kwa mabao 2 kwa 1.
Michuano ya nusu fainali ni siku ya Alhamisi, Barcelona watachuana na Guangzhou Evergrande ya China huku Sanfrecce Hiroshima ya Japan ikichuana River Plate kutoka Argetina.