Rais wa zamani wa Shirikisho la soka duniani FIFA Sepp Blatter, amesema amealikwa na rais wa Urusi Vladimir Putin, kuhudhuria fainali ya kombe la dunia mwaka 2018.
Blatter mwenye umri wa miaka 81, ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP kuwa, atahudhuria michuano hiyo licha ya kufungiwa kushiriki katika masuala la soka na FIFA.
Blatter aliongoza soka duniani kwa muda wa miaka 17, lakini ufisadi ulimwondoa katika uongozi wa soka duniani.
Licha ya mwaliko huo, Blatter amesema hajafahamu atahudhuria michuano hiyo kwa muda gani lakini anaamini kuwa, michuano hiyo itakuwa ya kufana.
Aidha, amesema kuwa rais Putin amemwalika aliyekuwa rais wa Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA Michel Platini.
Hata hivyo, mshirika wa karibu wa Platini amesema, kuwa kiongozi huyo wa zamani wa soka hajapokea mwaliko wowote kutoka kwa rais Putin.