Shrikisho la soka barani Afrika siku ya Jumatatu, litatangaza droo ya hatua ya makundi kuwania taji la Shirikisho barani Afrika baada ya kumalizika kwa michuano ya hatua ya mwondoano mwishoni mwa wiki iliyopita.
Klabu 16, zinatarajiwa kupangwa katika makundi manne kutafuta taji la mwaka 2019.
Klabu ya Gor Mahia ya Kenya, ndio timu pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki zilizofuzu katila hatua hiyo ya makundi baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya New Star ya Cameroon.
Ushindi wa wiki mbili zilizopita, uliisaidia Gor Mahia, kusonga baada ya kulazimisha sare ya kutofungana mwishoni mwa wiki iliyopita.
Gor Mahia imefuzu katika hatua ya makundi kwa mara ya kwanza, baada ya mwaka 2013 kuondolewa katika hatua ya kwanza, lakini 2012 na 2009 kuondolewa katika hatua ya awali.
Mbali na Gor Mahia, klabu zingine zilizofuzu ni pamoja na Etoile du Sahel, CS Sfaxien kutoka Tunisia, Raja Casablanca, RS Berkane na Hassania Agadir kutoka Morocco.
Klabu nyingine ni pamoja na AS Otoho ya Congo-Brazaville, Asante Kotoko ya Ghana, Enugu Rangers ya Nigeria, Petro de Luanda ya Angola, Salitas ya Burkina Faso.
Zambia itawakilishwa na Nkana na ZESCO United, huku Sudan ikiwakilishwa na Al-Hilal.