Klabu ya soka ya Simba FC imewafunga mahasimu wao wa jadi Yanga FC bao 1-0 katika mechi kali ya ligi kuu iliyochezwa Jumapili jioni katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Bao pekee la Simba lilifungwa na mchezaji Erasto Nyoni katika kipindi cha kwanza cha mchuano huo, ambao ulihudhiriwa na maelfu ya mashabiki wa Simba.
Simba ambayo mara ya mwisho ilishinda taji hili maara 2012, sasa inahitaji alama tano tu kutangazwa bingwa wa taji la msimu huu.
Klabu hiyo yenye makao yake katika mtaa wa Msimbazi Kariakoo, inaendelea kuongoza jedwali kwa alama 62.
Aidha, klabu hiyo haijafungwa mchuano wowote msimu huu hadi sasa.
Timu hizi mbili zimekuwa zikipambana tangu mwaka 1965. Mchuano wa kwanza kati ya timu hizi mbili, Yanga iliishinda Simba bao 1-0, wakati huo Simba ikiitwa Sunderland.
Licha ya kufungwa, kihistoria, Yanga wanaendelea kuongoza kwa ushindi dhidi ya Simba kwa sababu kwa nyakati zote wamekutana katika mechi za ligi kuu, imeshinda mara 38 huku Simba ikipata ushindi mara 28.
Yanga, ambayo imeshinda ligi ya soka Tanzania bara kwa misimu mitatu mfululizo, imekuwa ikiyumbayumba msimu hasa baada ya kuondoka kwa kocha wao George Lwandamina kutoka Zambia.
Klabu hiyo itawakilisha Tanzania katika michuano ya hatua ya makundi kuwania taji la Shirikisho barani Afrika.