Na Mwandishi Wetu kutoka Dar Es Salaam,
Simba SC Alhamisi hii ya Septemba 26 2019 itakuwa ugenini katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kucheza mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania bara dhidi ya Kagera Sugar “Wanakurukumbi”, Simba SC wanaenda kucheza mchezo huo wakiwa wana kumbukumbu ya kupoteza mchezo dhidi ya Kagera Sugar kwa magoli 2-1 msimu uliopita (Aprili 20 2019.
“Yaliyotokea msimu uliopita ni hamasa kwa wachezaji kufanya vizuri kwenye mchezo ujao na nimeshawaambia inabidi tuwaonyeshe mashabiki kwamba sisi ni Simba. Tunaenda na malengo ya kuhakikisha tunashinda” kocha Aussems kuelekea mchezo dhidi ya Kagera Sugar.
Simba SC wanarudi katika uwanja huo kupambana na Kagera Sugar iliyochini ya kocha Mecky Mexime ikiwa haijapoteza mchezp wowote msimu huu, ikiwa imecheza michezo mitatu na kushinda michezo yote mitatu, wakati Simba SC wakiwa wamecheza michezo miwili na kushinda yote.
Kagera Sugar anaongoza Ligi Kuu yenye timu 20 akiwa na alama 9 wakati Simba wapo nafasi ya tatu wakiwa na alama 6, timu ya Simba SC haina matokeo mazuri sana katika uwanja huo dhidi ya Kagera na mara yao ya mwisho kushinda ilikuwa msimu wa 2017/2018 waliposhinda kwa magoli 2-0.