Na Fadhili Omary Sizya,
Klabu ya Simba imesema inasubiri kupewa barua na Shirikisho la mpira wa miguu nchini Tanzania (TFF) inayoonyesha kweli wamepokwa pointi tatu za mchezo dhidi ya Kagera Sugar ili wakashitaki kwenye Mahakama ya usuluhishi ya FIFA (CAS) .
Simba ambayo ilipoteza mchezo huo mabao 2-1, ilikabidhiwa pointi tatu baada kamati ya usimamizi na uendeshwaji wa ligi (Kamati ya saa 72) kujiridhisha kuwa Kagera walimchezesha beki Mohamed Fakhi ambaye alikuwa na kadi tatu za njano kabla ya mchezo huo, pointi ambazo baadae zilirejeshwa kwa Kagera na kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo hii, Rais wa klabu hiyo Evans Aveva amesema hawawezi kukubali kuona timu yao inaonewa tena na TFF, hivyo kwa kuanzia wanasubiri wapewe barua ya kuporwa pointi tatu hizo ili wapeleke malalamiko yao CAS.
Hata hivyo Simba inaongoza ligi kuu bara ikiwa na pointi 59 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 56.