Na Paul Manjale,
SIMBA SC imerejea kileleni
mwa msimamo wa ligi kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya African Lyon jioni ya leo Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam.
Mshambuliaji Ibrahim Hajib alitangulia kuifungia Simba kwa shuti la mbali lililombabatiza beki wa Lyon, Hassan Isihaka na kutinga nyavuni dakika ya 37 baada ya kupokea pasi safi ya Muzamiru Yassin.
Bao hilo lilidumu kwa dakika nane pekee, kwani katika dakika ya 41,Omar Abdallah aliifungia African Lyon bao kuisawazishia kwa shuti kali la mbali lililomshinda kipa wa Simba Mghana, Daniel Agyei na kutinga wavuni.
Kipindi cha pili Simba walirejea tena juu ya mchezo kwa mara nyingine baada ya kufanikiwa kupata bao la pili katika dakika ya 54 baada ya beki wa African Lyon,Hamad Waziri kujifunga akiwa katika harakati za kuzuia mpira wa kichwa uliopigwa na Laudit Mavugo.
Ushindi huo umewafanya Simba wafikishe pointi 62 baada ya kucheza mechi 28.Pointi tatu mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 59 baada ya kucheza mechi 26.