Na Fredrick Nwaka Dar es Salaam,
Klabu za Simba, Yanga na Azam zinaendelea kupepetana katika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Baada ya michezo sita Simba ina alama 12 lakini inakaa kileleni mwa msimamo kwa kuwa ina magoli 15 ya kufunga ambayo ni mengi ikilinganishwa na wapinzani wao.
Yanga inakaa nafasi ya pili kwa kuwa ina magoli 5 ya kufunga wakati Azam inakaa nafasi ya tatu.
Simba ingeliweza kupanua uongozi wake kileleni lakini ilishindwa kuifunga Mtibwa Sugar na kutoka nayo sare ya bao 1-1.
Kagera Sugar ambayo msimu uliopita ilimaliza nafasi ya tatu inashika mkia ikiwa na alama mbili pekee.
Mchezaji wa zamani na Kocha wa timu hiyo, Mecky Maxime amesema msimuu huu una upinzani ikilinganishwa na msimu uliopita.
“Timu zimejipanga kila mmoja anataka matokeo, lakini ligi bado ni mbichi ninaamini tutarudi kwenye ushindani na kupata matokeo mazuri,”amesema nahodha huyo wa zamani wa Tinu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’