Benchi la ufundi la Simba limesema limejiandaa kikamifu kuhakikisha timu hiyo inaibuka na ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Majimaji.
Kesho, Simba itakuwa mwenyeji wa Majimaji ya Songea kwenye mchezo wa kukamilisha mzunguko wa kwanza utakaochezwa kwenye uwanja wa Uhuru, Mjini Dar es Salaam.
Kocha Msaidizi wa Simba Masoud Djuma amesema Simba haiwezi kudharau mchezo wowote ulio mbele yake na mipango yao ni kuhakikisha wanaibuka na alama tatu.
“Kila timu tunaipa uzito sawa, hatudharau mechi na ndio maana tunafanya mazoezi kwa nguvu zote na pia wachezaji wanapaswa kutambua thamani yao kwa Simba,”amesema Djuma ambaye alichukua mikoba ya ukocha msaidizi kutoka kwa Jackson Mayanja.
Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 32 baada ya kucheza mechi 14.
Leo mabingwa watetezi Yanga walioko kwenye nafasi ya tatu wanachuana na Azam katika mechi inayofanyika Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.