Klabu ya soka ya Simba SC kutoka Tanzania, imerejea katika hatua ya makundi kuwania taji la klabu bingwa barani Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 15.
Hatua hii ilikuja, baada ya klabu hiyo kuiondoa Nkana ya Zambia kwa kuwafunga mabao 3-1 katika mechi ya mzunguko wa pili iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es salaam.
Simba ilijihakikishia nafasi hiyo, katika dakika za lala salama baada ya Mzambia Clatous Chama, kuifungia klabu yake bao muhimu na kumaliza mchuano huo kwa ushindi wa mabao 4-3.
Mechi ya kwanza wiki iliyopita mjini Kitwe, Nkana walipata ushindi wa mabao 2-1.
Klabu nyingine kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zilizofuzu katika hatua hii uya makundi ni pamoja na mabingwa wa mwaka 2015, TP Mazembe kutoka DRC, walioishinda ZESCO United ya Zambia mabao 2-1.
AS Vita Club, pia imefuzu baada ya kuishinda Bantu FC ya Lesotho mabao 5-2 baada ya mechi za nyumbani na ugenini.
Droo ya hatua ya makundi inatarajiwa kutolewa tarehe 28 mwezi Desemba.
Klabu zilizofuzu ni pamoja na: Al-Ahly, Wydad Casablanca, Esperance de Tunis, Mamelodi Sundowns, Horoya, Club Africain, ASEC Mimosas, Orlando Pirates, CS Constantine, JS Saoura, Ismaily, Lobi Stars, FC Platinum.
Wakati uo huo, klabu 15 ambazo zitamenyana katika hatua ya mwondoano kutafuta timu zitakazofuzu katika hatua ya makundi, zimefahamika.
Hatua hii inakutanisha klabu zilizopata ushindi katika mechi za Shirikisho na zile zilizofungwa katika michuano ya klabu bingwa.
Miongoni mwa klabu hizo ni pamoja na ZESCO United, Al-Hilal, Gor Mahia, Nkana, Vipers, Zamalek, KCCA na Mukura Victory Sports.