Watani wa jadi katika mchezo wa soka, ligi kuu ya soka Tanzania bara, Yanga FC na Simba FC, wametoka sare ya bao 1-1 katika mchuano wa mzunguko wa kwanza kutafuta ubingwa msimu huu.
Mchuano huo uliochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam siku ya Jumamosi, ulihudhuriwa na maelfu ya mashabiki wa timu zote mbili ulijawa na hisia na mvutano hasa kipindi cha kwanza.
Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 26 kipindi cha kwanza kupitia mchezaji wa kimataifa kutoka Burundi Amis Tambwe.
Bao hilo lilizua utata huku kukiwa na madai ya Tambwe kuunawa mpira huo kabla ya kutikisa nyavu.
Mchezo ulisimamishwa kwa dakika kadhaa, huku mashabiki wa Simba wakivunja viti na kuvirusha uwanjani huku polisi wakilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kutuliza vurugu huku wengine wakiondoka kabisa uwanjani.
Baadaye, mchezo uliendelea lakini muda mfupi baadaye, nahodha wa Simba Jonas Mkude alioneshwa kadi nyekundu na kuiacha Simba ikiwa na wachezaji 10.
Kipindi cha pili, Simba walionekana kurejesha nidhamu na kujiamini zaidi na dakika chache kabla ya mchuanohuo kukamilika, Shiza Kichuya alipiga kona iliyojaa wavuni na kuisaidia Simba kuzawazisha katika mchezo huo.
Sare hii inaendelea kuiweka Simba kuendelea kuongoza kwa alama 17 baada ya mechi saba huku Yanga ikiwa ya tatu kwa alama 10.