Kampuni ya bahati nasibu kutoka Kenya ya Sportpesa imebisha hodi nchini Tanzania na kuzindua shughuli zake katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es salaam siku ya Jumanne katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Michezo nchini humo Harrison Mwakyembe na wadau wengine wa soka nchini humo.
Katika uzinduzi huo, timu ya taifa ya soka kwa vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys, imekuwa ya kwanza kufaidi baada ya Sportspesa kutoa ufadhili wa Dola 22,000 sawa na Shilingi za nchi hiyo Milioni 50 kusaidia timu hiyo.
Serengeti Boys wapo nchini Gabon kushiriki katika michuano ya bara Afrika itakayoanza tarehe 21 mwezi huu. Tanzania imepangwa katika kundi la B pamoja na Mali, Angola na Niger.
Waziri Mwakyembe amesema anatumai kungia kwa Sportpesa nchini Tanzania kutasaidia kuimarisha kwa soka katika taifa lake kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya.
Kampuni hii ndio inayofadhili ligi kuu ya soka nchini Kenya na kufadhili timu za AFC Leopards na Gor Mahia.
Mkurugenzi wa Sportspesa nchini Tanzania Abbas Tarimba kwa upande amesema kuwa wamefuatilia kwa karibu mafanikio ya soka nchini Kenya ambayo sasa yanakuja Tanzania.
Kampuni hii inatarajiwa pia kufadhili timu ya Simba na Yanga na kuendeleza miradi mbalimbali ya soka nchini humo katika siku zijazo.
Sportspesa pia inashirikiana na ligi kuu ya soka nchini Uhispania lakini pia inafadhili klabu ya Hull City inayoshiriki katika ligi kuu ya soka nchini Uingereza.