Na Victor Abuso.
Klabu ya Stand United yenye makao yake mjini Shinyanga Kaskazini mwa Tanzania imemsajili Kiungo wa kati wa zamani wa Yanga FC Hassan Dilunga.
Deokaji Makomba, msemaji wa klabu hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia , amesema mchezaji huyo amesaini mkataba wa mwaka mmoja.
Pamoja na Dilunga, klabu hiyo imemsajili pia Amri Kiemba na wachezaji hao sasa wanatarajiwa kujiunga na wenzao katika kambi yao mjini Kahama.
Kabla ya kusajiliwa na klabu yake mpya, Kiemba alikuwa anaichezea Azam FC lakini pia amewahi kuichezea Yanga na Simba kwa nyakati tofauti.
Usajili huu unakuja siku kadhaa baada ya Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF, kuongeza muda wa kufungwa kwa dirisha la usajili wa wachezaji wanaocheza katika ligi kuu ya soka Tanzania bara.
Siku ya mwisho ya kuwasajili wachezaji hao itakuwa siku ya Alhamisi juma hili.
Muda wa mwisho ulikuwa unatarajiwa kufungwa tarehe 6 mwezi huu huku ule usajili mdogo wa ndani ungefungwa Septemba tarehe 5 na sasa usajili wa ujumla utamalizika tarehe 20.
Uongozi wa soka nchini humo umeongeza kuwa kati ya tarehe 21 na 28 utakuwa ni kipindi cha pingamizi.
Ligi kuu ya Tanzania bara inatarajiwa kuanza mwezi Septemba.