Timu ya taifa ya soka ya Sudan Kusini huenda ikakosa mchuano wake wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Equitorial Guinea mwishoni mwa wiki hii kufuzu katika michuano ya mataifa bingwa barani Afrika itakayofanyika mwaka 2017 nchini Gabon.
Hii ni kutokana na mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini humo ambao umekwamisha shughuli mbalimbali katika taifa hilo changa zaidi duniani.
Baraza la Mawaziri nchini humo na bunge bado halijajadili na kupitisha bajeti ya timu hiyo inayotarajiwa kusafiri kwenda jijini Malabo.
Mchuano huo umepangwa kufanyika siku ya Jumapili katika uwanja wa Estadio di Malabo.
Timu ya Sudan Kusini inayofahamika kwa jina maarufu la Bright Stars wanashikilia nafasi ya tatu katia kundi C nyuma ya Mali na Benin.
Shirikisho la soka nchini humo SSFF limesema hadi sasa halina fedha ya kwenda nchini Equitorial Guinea licha ya kuomba msaada kutoka serikalini.
Ikiwa Sudan Kusini itakosa mchuano huo, itachukuliwa hatua na Shirikisho la soka barani Afrika CAF kwa kutozwa faini.