Timu ya taifa ya soka ya Sudan imemaliza katika nafasi ya tatu katika michuano ya CHAN biana ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani, inayomalizika Jumapili, nchini Morocco.
Sudan imeshinda medali ya shaba katika mashindano hayo baada ya kuishinda Libya mabao 4-2 baada ya kupigwa kwa mikwaju ya penalti.
Mchuano huo ulikwenda katika hatua hiyo baada ya sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida na ule wa ziada.
Huu ni ushindi mkubwa kwa Sudan inayofunzwa na kocha kutoka Croatia Zdravko Logarusic na matokeo haya yamewashangaza wengi ambao hawakuipa nafasi ya kufanya vizuri katika mashindano haya.
Sudan ilianza mchuano huo kwa kupata bao la ufunguzi katika dakika ya nane ya mchuano huo kupitia mshambuliaji Walaaeldin Musa na kuonekana kutawala mchuano huo hadi dakika 84, wakati waliporuhusu Libya kusawazisha kupitia Salem Ablo, aliyefunga kwa kichwa.
Libya ilishinda taji la CHAN mwaka 2014, wakati michuano hii ilipoandaliwa nchini Afrika Kusini.
Mbali na mchuano huu, wenyeji Morocco watamenyana na Nigeria katika fainali ya mchuano huu utakaopigwa katika uwanja wa Mohammed V mjini Casablanca.
Mshindi katika fainali hii atajishindia taji na Dola za Marekani Milioni 1.25.