Timu ya taifa ya soka ya Tanzania Taifa Stars itamenyana na The Fox Desert ya Algeria tarehe 14 mwezi wa Novemba katika mchuano wa nyumbani hatua ya pili kufuzu kwa fainali za kombe Dunia zitakazofanyika mwaka 2018 nchini Urusi.
Mchuano huo utachezwa katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam kabla ya ule wa marudiano tarehe 17 mwezi huo wa Novemba jijini Algers.
Rais wa Tanzania akizungumza juma hili jijini Dar es salaam, ametoa wito kwa wachezaji wa Taifa Stars kujikakamua ili kuishinda Algeria nyumbani na ugenini ili kusonga mbele.
Kikwete amewaambia wachezaji wa Stars kuwa kazi kubwa ipo mbele yao.
Taifa Stars itapiga kambi nchini Afrika Kusini kwa siku 10 kuanzia tarehe 3 mwezi huu kabla ya kurejea jijini Dar es salaam kuikabili Algeria.
Taifa Stars ilifanikiwa kusonga mbele katika hatua ya pili ya michuano hiyo baada ya kuifunga Malawi kwa jumla ya mabao 2-1, nyumbani ikishinda 2-0, na kufungwa 1–0 jijini Blantyre mwishoni mwa juma lililopita.