Na Victor Abuso,
Waziri wa michezo nchini Tanzania Fenella Mukangara ametoa wito kwa wachezaji wa soka nchini humo kujitolea na kutia bidii ili kupata matokeo mazuri katika michuano ya Kimataifa.
Akijibu maswali ya wabunge kuhusu matokeo mabaya ya Taifa Stars ambayo mwishoni mwa juma lililopita ilifungwa na Uganada mabao 3 kwa 0 katika mchuano wa kufuzu katika fainali za CHAN mwakani, Waziri huyo amesisitiza kuwa wakati kocha Mart Nooij akiteuliwa kulikuwa na matumaini kuwa ataisadia timu.
“Wakati TFF ikimpa kazi, tulifahamu kuwa ni kocha makini ambaye atatusaidia kupata ushindi katika michuano mbalimbali,” aliwaambia wabunge jijini Dodoma siku ya Jumatatu.
Waziri Mukangara ameongeza kuwa kwa sasa serikali inashirikiana na TFF ili kumpata kocha mpya atakayeiongoza Tanzania katika michuano ya Kimataifa ikiwemo ile ya kufuzu katika fainali za Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.
“Tunazugumza na TFF, kuona kuwa tunampata kocha mwingine kuisaidia Tanzania lakini pia natoa wito kwa wachezaji kujitolea ili kupata matokeo mazuri,” aliongeza.
Baada ya Tanzania kufungwa na Uganda mwishoni mwa juma lililopita visiwani Zanzibar, rais wa TFF Jamal Malinzi aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa wameachana na kocha Nooij raia wa Uholanzi.
Kamati kuu ya TFF mapema mwezi huu ilimpa nafasi ya mwisho kocha Nooij kuisaidia Tanzania kufuzu katika michuano ya CHAN itakayofanyika nchini Afrika Kusini mwakani la sivyo watamwachisha kazi.
Tangu kumalizika kwa michuano ya COSAFA baina ya timu za Kusini mwa Afrika ambako Tanzania ilipoteza michuano yake yote, kumekuwa na shinikizo kutoka kwa mashabiki kuwa kocha afutwe kazi.
Mart Nooij alianza kazi ya ukufunzi barani Afrika mwaka 2003 kwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana wasiozidi miaka 20, kati ya mwaka 2007 na 2011 alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Msumbiji, mwaka 2012 aliifunza klabu ya Santos Cape Town kabla ya kuhamia Saint George ya Ethiopia kati ya mwaka 2013 na 2014.
Tanzania ilimwajiri mwaka uliopita na kumfuta kazi mwishoni mwa juma lililopita.