Na Victor Abuso
Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) ipo katika maandalizi ya dakika za lala salama kabla ya kuingia dimbani kuwania ubingwa wa taji la soka baina ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika COSAFA inayoanza siku ya Jumapili nchini Afrika Kusini.
Kocha mkuu wa timu ya Taifa Stars Mart Nooij amesema vijana wake wanaendelea vizuri na mazoezi, na ana matumaini makubwa kuwa watafanya vizuri katika makala haya ya 15 ya michuano hii mikubwa Kusini mwa Afrika.
Aidha, kocha huyo ameonekana kufurahia makaribisho na uwanja wanaotumia kufanyia mazoezi na kusisitiza kuwa kikosi chake kipo tayari kwa kazi iliyo mbele yao.
Tanzania ipo katika kundi la B pamoja na Lesotho, Madagascar na Swaziland na mchuano wake wa kwanza ni Jumatatu dhidi ya Swaziland katika uwanja wa Royal Bafokeng.
Mara ya mwisho kwa Stars kukutana na Swaziland ilikuwa ni mwaka uliopita katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki na kutoka sare ya bao 1 kwa 1.
Licha ya kusaka ubingwa huo, Tanzania ambao ndio wawakilishi wa pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati katika michuano hiyo, wanatumia michuano hii kwa maandalizi ya michuano ya kufuzu kutafuta kushiriki katika michuano ya Afrika mwaka 2017 itakayoanza mwezi Juni.
Mbali na Tanzania, mataifa mengine yanayoshiriki katika hatua ya makundi katika michuano hii ni pamoja na Namibia, Mauritius, Ushelisheli na Zimbabwe.
Mshindi wa kila kundi atafuzu katika hatua ya robo fainali na kuungana na wenyeji Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia, Ghana, Bostwana na Malawi.
Mchuano wa kwanza wa robo fainali utachezwa tarehe 24 mwezi huu kati ya Ghana na mshindi wa Kundi la B.
Fainali ya michuano hii itapingwa tarehe 30 mwezi huu.