By Fadhili Omary Sizya,
Ligi kuu Tanzania bara inazidi kushika kasi, mechi kadhaa zikiwa zinaendelea leo hii na wababe Mbao Fc baada ya jana kwenda suluhu na Singida United wamesalia kileleni kwenye msimamo wa TPL.
Kagera Sugar Vs African Lyon (Kaitaba Stadium)
African Lyon chini ya kocha raia wa Ufaransa Soccoia Lionel wameanza kwa kusuasua msimu wao wa kwanza tangu warejee ligi kuu, wakicheza mechi mbili na kuambulia alama moja pekee, hivyo watakuwa na kazi ya kuizuia Kagera katika uwanja wao wa nyumbani.
Kocha Meck Mekxime ameonekana kuirejesha upya Kagera Sugar, mchezo wa pili tangu washinde 2-1 dhidi ya Mwadui, huku akiwa hana mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake ,timu hiyo inaonekana kuwa na morali kubwa sana.
Coastal Union vs Kmc (Ccm Mkwakwani)
Wote ni wageni katika michuano ya ligi kuu, Coastal wamerejea msimu huu na Kmc ni mara ya kwanza kucheza Tpl.
Coastal ni timu pekee inaweza kuifikia kileleni Mbao Fc endapo itashinda katika mchezo huo, Juma Mgunda kocha mkuu wa Coastal amethibitisha uwepo wa mshambuliaji mpya Ally Kiba kutumika katika mchezo huo.
Kmc wao chini ya Etienne Ndayiragije anakiongoza kikosi hicho kipya katika mechi ya tatu akiwa na kumbukumbu ya sare mbili za awali, upande ya hali ya timu alisema hana majeruhi kikosini kwake.
Mtibwa Sugar vs Mbeya City (Manungu Complex)
Mbeya City hawajaanza vyema msimu huu, wamepoteza mechi zote mbili za awali ligi kuu, tofauti na Mtibwa ambao walijipanga tangu waanze kwa kichapo bao 2-1 dhidi Yanga wameibua matumaini kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Prisons.
Hii ni mechi ngumu kwa Mbeya City,mechi zao zote tatu wameanzia ugenini na imeipa tabu klabu hiyo kupata ushindi.
Stand United vs Biashara United (Ccm Kambarage)
Stand wanaikaribisha Biashara timu ngeni kwa mara kwanza Tpl lakini tayari walianza kuonyesha ubora baada ya kuichapa 1-0 Singida United.
Msimu uliopita kwa Stand walionekana kuwa imara sana, msimu huu wameanza kwa kusua sua na mchezo wa mwisho dhidi ya Mbao walifungwa 2-1.
Tanzania Prisons vs Alliance Fc (Kumbukumbu ya Sokoine)
Prisons hawana utofauti na Mbeya City, timu hizi kutoka mkoa mmoja zimeanza kwa kupoteza mechi zao za awali wakifuatana chini kabisa msimamo wa TPL.
Timu hizi zinakutana mchezo huu kwa uwiano mkubwa aina ya uchezaji wao unafanana, wakicheza soka la kutulia, pasi fupi fupi, kandanda la kuvutia sana kwenye mechi hiyo.
Alliance ni timu mpya TPL wametoa sare 1-1 mchezo wa mwisho dhidi ya African Lyon ili kuleta matumaini ya kusalia ligi kuu itabidi wapambane kushinda mchezo huu.