Timu ya taifa ya mchezo wa soka ya Tanzania Taifa Stars, imekuwa na mwaka mgumu viwanjani mwaka 2015.
Shirikisho la soka nchini humo lilikuwa na matumaini kuwa Taifa Stars iliyofuzu mara ya mwisho katika mashindano ya mataifa bingwa barani Afrika mwaka 1980, ingefanikiwa kucheza katika fainali za mwaka huu nchini Equatorial Guinea.
Taifa Stars ikifunzwa na Mholanzi Mart Nooij ilishindwa kufika katika hatua ya makundi na kampeni yake kufikia mwisho katika mzunguko wa pili baada ya kufungwa na Msumbiji kwa jumla ya mabao 4 kwa 3.
Mchuano wa kwanza uliochezwa katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam, wenyeji Tanzania walitoka sare ya mabao 2 kwa 2 na kupoteza mchuano wa marudiano baada ya kufungwa kwa mabao 2 kwa 1.
Wachambuzi wa soka nchini humo walisema kukosekana kwa umakini wa wachezaji wa Taifa Stars ulisababisha kuondolewa mapema katika kampeni ya kwenda nchini Equatorial Guinea.
Kufutwa kazi kwa kocha Mart Nooij.
Kocha Mart Nooij aliyepewa kibarua cha kuifunza Taifa Stars mwaka 2014 baada ya kutokea nchini Msumbuji, alifutwa kazi mwezi Juni.
Tanzania chini ya kocha Nooij ilipoteza mechi kadhaa za kimataifa na ikawa sababu ya kufutwa kazi.
Miongoni mwa michuano ambayo Tanzania ilipoteza chini ya kocha huo ni dhidi ya Misri ilipofungwa mabao 3 kwa 0 kutafuta nafasi ya kufuzu kucheza fainali za kombe la mataifa bingwa barani Afrika mwaka 2017 nchini Gabon.
Uganda pia iliilemea Tanzania kwa kuwashinda mabao 3 kwa 0 mwezi Juni visiwani Zanzibar katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za taji la Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani, michuano itakayofanyika mwaka 2016 nchini Rwanda.
Matokeo mengine mabaya ya Tanzania yaliyoendelea kumpa wakati mgumu kocha Nooij ni wakati Taifa Stars ilipofungwa na Swaziland bao 1 kwa 0, ikalemewa na Madagascar mabao 2 kwa 0, ikapoteza bao 1 kwa 0 dhidi ya Lesotho na wakiwa jijini Kigali nchini Rwanda walifungwa mabao 2 kwa 0 katika mechi za kimataifa za kirafiki.
Hisia za kocha Nooij baada ya kufutwa kazi.
Mwishoni mwa mwezi Juni, rais wa Shirkisho la soka TFF Jamal Malinzi alitangaza hatua ya kumfuta kazi kocha Nooij.
Kabla ya kuchukuliwa hatua hiyo, rais wa TFF alifanya kikao na Kamati kuu ya Shirikisho hilo na kumpa nafasi ya mwisho kwa kocha huyo kuifunga Uganda na kufuzu katika michuano ya CHAN lakini kwa bahati mbaya hilo halikufanyika.
Kocha Nooij, alikubali hatua ya TFF na kuwashukuru viongozi wa soka nchini humo kwa kumpa nafasi ya kuifunza Taifa Stars.
Nooij alisema hakupata matokeo mazuri kwa sababu kikosi chake cha vijana chipukizi hakikuwa na uzoefu wa kucheza mechi za kimataifa.
Mart Nooij aliamini sana falsafa ya kuwapa vijana nafasi kuonesha uwezo wao katika michuano ya kimataifa.
Kuajiriwa kwa kocha Boniface Mkwasa.
Baada ya kumfuta kazi kocha Mart, uongozi wa TFF ulimteua naibu kocha wa Yanga Boniface Mkwasa kuchukua nafasi hiyo.
Mchuano wake wa kwanza ulikuwa wa marudiano dhidi Uganda kufuzu katika michuano ya CHAN jijini Kampala na kutoka sare ya mabao 1 kwa 1.
Mwezi Oktoba katika michuano ya kufuzu kwa kombe la dunia, Taifa Stars ilifungwa na Malawi bao 1 kwa 0 huku matokeo mabaya yakiwa ni kufungwa mabao 7 kwa 0 na Algeria mwezi Novemba.
Michuano ya CECAFA iliyofanyika nchini Ethiopia, kati ya mwezi Novemba na Desemba ilifika katika hatua ya robo fainali na kuondolewa na wenyeji Ethiopia.
Tanzania iliifunga Somalia mabao 4 kwa 0 huku ikiishinda Rwanda mabao 2 kwa 1.
Tanzania inaendelea na kampeni ya kutafuta tiketi ya kufuzu kwa kombe la dunia itakayofanyika nchini Urusi mwaka 2018.
Mwezi Machi watamenyana na Chad jijini D’jamena na kurudiana na Nigeria ugenini baada ya kutoka sare ya kutofungana nyumbani mwezi Septemba jijini Dar es salaam.
Wachezaji muhimu
Wachezaji waliovuma mwaka huu ni pamoja na washambuliaji Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na John Bocco bila kumsahau nahodha Nadir Haroub.