Connect with us

 

Timu ya taifa ya soka ya Ghana yenye umri chini ya miaka 17, itamenyana na Niger katika hatua ya nusu fainali kuwania ubingwa wa bara Afrika, katika michuano inayoendelea nchini Gabon.

Mechi hiyo itachezwa siku ya Jumatano katika uwanja wa Port-Gentil.

Nusu fainali ya pili, itaikutanisha mabingwa watetezi Mali na Guinea katika uwanja wa l’Amitie jijini Libreville, mechi ambayo pia itachezwa siku ya Jumatano.

Ghana ilifuzu baada ya kuongoza kundi A kwa alama 7, kwa kushinda mechi 2 na kwenda sare mechi 1,huku Guinea ikimaliza ya pili kwa alama 5 baada ya kushinda mechi 1 na kwenda sare michuano miwili.

Mali nayo ilifuzu baada ya kumaliza ya kwanza kwa alama saba, baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare mara moja. Mali haikupoteza mechi hata moja.

Niger ilifanikiwa kufuzu katika hatua hiyo baada ya kushinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Tanzania kwa kuifunga bao 1-0 na kumaliza wa pili katika kundi lake kwa alama 4.

Licha ya Tanzania kuwa na alama 4, sawa na Niger, haikufanikiwa kusonga mbele kwa sababu ya wingi wa mabao, ilikuwa na mabao 2  huku Niger ikapata mabao 4, matokeo ambayo yameihuzunisha Tanzania.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufuzu na kushiriki katika michuano hii, na licha ya kupoteza katika mchuano wake wa mwisho, wachambuzi wa soka wanasema kikosi hicho kina nafasi kubwa ya kufanya vema katika michuano ijayo.

Licha ya kufuzu katika hatua ya nusu fainali, mataifa hayo manne yatawakilisha bara la Afrika katika michuano ya kombe la dunia mwezi Oktoba nchini India.

More in